Thursday, 17 May 2018

Dk Kebwe afanya ziara ya kushtukiza kwenye maghala ya mafuta ya kula


Dk. Kebwe Stephen akiwa katika moja ya maghala hayo ya kuhifadhia mafuta ya kupikia.


MKUU wa mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen amefanya ziara ya kushtukiza  kwenye maghala ya kuhifadhi mafuta ya kula na sukari katika mkoa wake ili kubaini wafanyabiashara wanaoficha bidhaa hiyo.

Dk. Kebwe amefanya ziara hiyo juzi Mei 15,2018  akiambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo ambapo walibaini maghala mengi yakiwa na mafuta ya kula na kuwataka wafanyabiashara hao kupeleka sokoni kuyauza kwa bei elekezi ya Serikali. 

Hata hivyo, DK. Kebwe amekemea vikali kitendo cha wafanyabiashara hao kuchanganya bidhaa za chakula kama mafuta ya kula na sukari na bidhaa nyingine kama sabuni chumvi n.k zikiwa ghala moja kwa kuwa kufanya hivyo kunahatarisha afya ya walaji.
 
Wakati wa ukaguzi huo, Dk. Kebwe ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, amemuagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro na moafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wa mkoa huo kummhoji mfanyabishara wa mafuta ya kula,  Hussein Bionzo na kupitia nyaraka zake za biashara ili kujiridhisha iwapo analipa kodi stahiki serikalini. 

Hatua hiyo imekuja baada ya makosa kadhaa yaliyojitokeza wakati wa mchakato huo wa  kukagua bidhaa ya mafuta ya kula katika ghala lake.

Katika hatua nyingine Dk. Kebwe amewataka wananchi wa Morogoro kutokuwa na wasiwasi kuhusu bidhaa ya mafuta kwa kuwa ipo ya kutosha huku akiwataka wakuu wa wilaya wa mkoa huo kupita katika maduka ya reja reja na kusimamia bei elekezi kwani huko ndiko kuna tatizo la kupandisha bei hasa wakati huu wa kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

No comments:

Post a Comment