Monday, 7 May 2018

Kibaha kufanya maonesho ya ujasiriamali Agosti

Katibu wa jukwaa la uwezeshaji wanawake mkoani Pwani, Elina Mgonja, akizungumza wakati wa sherehe za kukabidhi tuzo ya mwanamke bora 2018 Tanzania kwa mkoa huo.


Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama (kulia), akikabidhiwa tuzo ya mwanamke bora 2018 Tanzania ya ushindi wa tatu kwa mkoa wa Pwani,waliyoshinda katika mashindano ya Taifa, wa kwanza (kushoto) Katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji wanawake mkoani Pwani, Elina Mgonja na katikati ni mwenyekiti wa jukwaa hilo, Jovita Masanyika. (PICHA NA MWAMVUA MWINYI)


Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama akionesha tuzo ya mwanamke bora 2018 Tanzania ya ushindi wa tatu kwa mkoa wa Pwani, waliyoshinda katika mashindano ya Taifa .(PICHA NA MWAMVUA MWINYI) 


Mwamvua Mwinyi, Kibaha

WILAYA Kibaha, mkoani Pwani inatarajia kuanzisha maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiriamali kuanzia Agosti mwaka huu ili kuwasaidia kujitangaza na kupata soko.

Mkuu wa wilaya hiyo, Assumpter Mshama amebainisha suala hilo wakati wajasiriamali wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake mkoani Pwani, walipomkabidhi tuzo ya mwanamke bora 2018 Tanzania ya ushindi wa tatu kwa mkoa huo.

Amesema wametenga maeneo kwa ajili ya kufanya maonesha hayo ambayo lengo ni kuhakikisha yanafanyika kila mwezi kwa wajasiriamali ambao watatangaza biashara zao.

“Mmepiga hatua kubwa katika kuhifadhi na kutengeneza bidhaa zenu, lakini mkumbuke kuzalisha bila mauzo wala kupata soko ni kazi bure,”amesema Mshama.

Ameongeza kuwa mafanikio yanayopatikana kwa wajasiriamali wa wilaya na mkoa huo yanatokana na ushirikiano baina yao na serikali na halmashauri kuwawezesha wanawake na vijana.


Mshama amewataka wanawake kuacha kuwa wabinafsi na badala yake wajiunge kwenye majukwaa ya uwezeshaji na makundi ili waweze kusaidiwa kirahisi.

Mkuu huyo wa wilaya amesema wakati umefika kwa wanawake wajasiriamali kukimbilia fursa, kujikubali, kujiamini na kuthubutu ili kujiinua kimaendeleo na kuacha utegemezi ndani ya familia.

Mshama amewaasa kuacha kuigana kufanya biashara moja na badala yake kila mmoja awe mbunifu kuangalia fursa ya biashara itakayomlipa.

“Hakuna mtu ama mjasiriamali mmoja mmoja atakayepewa fedha hiyo mkononi bila utaratibu wowote ” Hivyo mjiunge muweze kuwezeshwa kirahisi,” amebainisha.

Aidha amewapongeza kwa kujinyakulia tuzo kwenye mashindano ya Taifa yaliyofanyika mkoani Dodoma hivi karibuni.

Katibu wa jukwaa hilo mkoani Pwani ambae pia ni diwani wa viti maalum, Elina Mgonja amesema mkoa huo wa viwanda watahakikisha wanawapatia mafunzo wajasiriamali ili waweze kuwa na viwanda vidogo vidogo.

Ameishukuru serikali na halmashauri kwa kujali kundi la wanawake na vijana wa kike walio kwenye vikundi na kuitaka izidi kuwawezesha mikopo.

Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Jovita Masanyika ameiomba Serikali iangalie suala la riba kwa taasisi za kifedha ili kuwapunguzia makali wajasiriamali mbalimbali mkoa, wilaya na Taifa kijumla.

No comments:

Post a Comment