Saturday, 5 May 2018

Kutofanya ngono katika umri mdogo kunazuia saratani - Dk Mwaiselage


Dk. Julius Mwaiselage

Claudia Kayombo

SARATANI ya shingo ya kizazi ni moja kati ya aina hatari za maradhi ya saratani inayoweka rehani maisha ya wanawake wengi nchini na duniani kote.

Wataalamu wa tiba wanabainisha umri ambao ni hatari kwa mwanamke kukumbwa na maradhi ya saratani ya shingo ya kizazi kuwa ni kati ya miaka 20 na 39.

Hata hivyo, mwanamke anaweza kukumbwa na saratani hiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania, hata baada ya umri huo.

Takwimu za mwaka 2010 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), zinasema Tanzania ina wastani wa wanawake 6,241, wanaougua saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka, huku 4,355 miongoni mwao wanapoteza maisha.

Takwimu hizo zinaongeza hamasa kuwa ipo haja kwa serikali, mashirika na wadau mbalimbali kuweka mikakati ya makusudi ili kuwanusuru wanawake katika hatari ya kukumbwa na maradhi haya hatari yasiyotibika yakichelewa kugunduliwa.

Aidha, ripoti nyingine ya WHO, inasema saratani hiyo ni ya nne inayoongoza kwa kusababisha vifo vya  wanawake katika nchi zinazoendelea.

Ripoti ya mwaka 2012 ya shirika hilo, inasema kati ya matukio 75,000 ya waathirika wa saratani ya kizazi, 50,000 yametokea barani Afrika.

Hata hivyo, takwimu zilizotolewa mwaka jana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wagonjwa waliolazwa katika taasisi hiyo ni wanawake na wengi wao wanakabiliwa na saratani hiyo.

Aina hii ya saratani inawaathiri watu wa tabaka zote, na inashika nafasi ya pili duniani miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake.

Wagonjwa wapya 529,828 wanagundulika kuugua maradhi hayo kila mwaka duniani, huku asilimia 85 miongoni mwao wakitoka nchi zinazoendelea.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage anasema saratani ya shingo ya kizazi inaongoza miongoni mwa saratani zote nchini kwa kuwa ina asilimia 40 ya wagonjwa wote wanaougua aina mbalimbali za saratani nchini.

Dk. Mwaiselage anataja moja ya vyanzo vya saratani hiyo kuwa ni kuanza kufanya ngono mapema na kwamba wasichana wanaowahi kuanza vitendo hivyo wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.

“Saratani ya shingo ya kizazi hapa nchini inaongoza kwa asilimia 40 ikifuatiwa na ya ngozi kwa asilimia 20, saratani ya matiti ni ya tatu ina asilimia 12 ya wagonjwa na ya njia ya koromea ni kwa asilimia tisa,” anasema.

Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa baada ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitisha mwongozo wa tiba shufaa, kinachoendelea ni kuhakikisha kila hospitali nchini inatoa tiba hiyo.

“Tunashirikiana na wadau mbalimbali kikiwemo Chama cha Tiba Shufaa (TPCA), kuhakikisha huduma hii inapatikana hadi kwenye ngazi ya zahanati hapa nchini,” anasema.

Dk. Mwaiselage anafafanua kuwa wagonjwa wa saratani wanapitia katika hatua nne ambazo ni mtu kutibiwa na kupona, hatua ya pili anaweza kupona kwa asilimia 50, wakati hatua ya tatu na ya nne mgonjwa anakuwa na kiwango cha juu cha maumivu hivyo anahitaji tiba shufaa ambayo ni muhimu kwake.

"Kwa ujumla tiba shufaa inatumika kwa wagonjwa wa muda mrefu ambao wamekata tamaa, inawaondolea maumivu makali na kuwafanya wawe na matumaini makubwa hata kama hawawezi kupona,” anasema.

Mkuu wa Idara ya Kinga wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa anasema saratani ya shingo ya kizazi ni aina ya saratani inayoshambulia seli zilizoko ndani ya ngozi laini inazunguka shingo ya kizazi.

Anasema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya saratani ya shingo ya kizazi inasababishwa na kirusi kinachoitwa Human Papilloma Virus (HPV), ambacho kinaenea kwa njia ya kujamiiana.

“Saratani ya shingo ya kizazi inachukua nafasi kubwa kwa kinamama na hapa Ocean Road ndipo saratani hii inaongoza kwa wanawake,”anasema Dk. Kahesa.

Aidha, mtaalamu huyo wa afya anataja tabia ambazo zinachangia mtu kupata saratani ya shingo ya kizazi ni pamoja na wasichana kuanza ngono wakiwa na umri mdogo.

Dk. Kahesa anasema tabia nyingine hatarishi ni kujamiiana na mwanaume mwenye wapenzi wengi ambapo anakuwa katika uwezekano wa kusambaza kirusi hicho iwapo mmoja wa wanawake anaohusiana nao wanakabiliwa na saratani ya shingo ya kizazi.

Pia uvutaji wa sigara nao unamweka mwanamke katika hatari ya kukabiliwa na maradhi hayo, kwa kuwa kemikali iliyo katika moshi wa sigara inasababisha ugonjwa huo.

Anataja kemikali ya benzini ambayo inasafirishwa kwa njia ya damu kuwa inaweza kusababisha saratani sehemu yoyote ikiwemo ya shingo ya kizazi katika mwili wa binadamu.

Dk. Kahesa anataja tabia nyingine hatarishi ni matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula au kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi, kutokula mboga za majani na matunda na upungufu wa kinga mwilini.

“Shida hivi vitu havikai kimoja kimoja, mvutaji sigara huyo huyo anafanya uasherati na hatari inaongezeka kunapokuwa visababishi vingi,” anasisitiza.

Dk. Kahesa anafafanua kuwa saratani ya shingo ya kizazi inaweza kuanza na kukaa kwa muda mrefu bila kuonesha dalili yoyote na kwamba wakati mwingine inapokuja kuonekana ugonjwa unakuwa katika hatua za mwisho.

Miongoni mwa dalili za saratani ni kutoka damu isiyo ya kawaida ukeni, kutokwa na damu ukeni baada ya kujamiiana na au kutokwa na damu ukeni kwa wanawake waliokoma hedhi.

Dakta Kahesa anasema dalili nyingine ni kutokwa na damu ukeni iliyo na majimaji ya uke, matone ya damu au damu kutoka kipindi ambacho siyo cha hedhi, kutokwa na majimaji au uchafu ukeni wenye harufu mbaya na wakati mwingine unakuwa umechanganyika na damu.

Hali kadhalika mtu anaweza kupata maumivu wakati wa kujamiiana, maumivu chini ya tumbo, nyonga na kiuno, kukojoa mkojo wenye damu, kupitisha mkojo na haja kubwa kwenye uke na upungufu wa damu.

Anafafanua kuwa mtu anaweza kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi kwa kuepuka ngono katika umri mdogo, kuwa na mwenzi mwaminifu, kuepuka kuvuta sigara, kupima mara kwa mara saratani japo mara moja kwa mwaka, kupata chanjo ya ‘Human Papilloma Visur’ na kuepuka kula vyakula vyenye mafuta mengi.

No comments:

Post a Comment