Wednesday, 2 May 2018

Mkikita yatoa unga tani 1.7 kusaidia watoto yatimaMwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita), Dk.Kissui Kissui na Mkurugenzi wa Mkikita, Adam Ngamange, wakimkabidhi msaada wa unga wa muhogo Mwanzilishi wa Kituo cha kulelea yatima cha Hananasifu (Hocet), Hezekia Mwalugaja na baadhi watoto wanaolelewa kituoni hapo. (PICHA NA SULEIMAN MSUYA)

Suleiman Msuya

MTANDAO wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita), umetoa msaada wa unga wa muhogo tani 1.7 zenye thamani ya sh. mil. 3.5 kwa kituo cha kulea watoto yatima Hananasifu (Hocet).

Msaada huo wa unga umekabidhiwa kwa Hocet na Mwenyekiti wa Bodi ya Mkiita, Dk. Kissui Kissui jana jijini Dar es Salaam.

Amesema wameamua kusaidia kituo hicho kama sehemu ya mchango wao kwa jamii na kwamba kiasi hicho ni sehemu ya mavuno ya kwanza ya uwekezaji wao katika kilimo hicho.

Dk. Kissui amesema Mkikita wamelima muhogo katika  maeneo ya Bagamoyo, Mkuranga na Kisarawe.“Tumelima muhogo katika mashamba yetu tumevuna na baada ya kusaga tumepata tani 15 hivyo tumekubaliana kutoa tani 1.7 Hocet ili vijana waweze kupata chakula kwa siku chache kwani ni wadau wetu,” amesema.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa pamoja na msaada huo wa chakula kwa Hocet wanaamini kuwa kupitia wao watakuwa wamefikisha ujumbe kwa jamii kuhusu kufanya kilimo chenye tija zaidi.

Mkurugenzi wa Mkikita, Adam Ngamange amesema wametoa msaada huo kwa kituo cha watoto yatima wakiamini kuwa ni sehemu sahihi hata kwa maagizo ya Mungu.

“Mungu ameagiza yatima wasaidiwe na sisi katika mavuno yetu ya kwanza tangu kuanza kuwekeza wenyewe tumeona tuanze na vijana hawa ambao wanahitaji msaada na biashara itafuata,” amesema.

Ngamange amewataka wakulima nchini kutumia Mkikita katika kutafua masoko ya bidhaa zao kwani uhakika wa kupata soko ni mkubwa kutokana na mtandao waliona duniani.

Amesema Mkikita inajihusha na kilimo cha muhogo, papai, pilipili kichaa na mazao mengine ambayo yamekuwa yakihitajika katika nchi mbalimbali kama China, Uturuki na Ujerumani.

Mwanzilishi wa Hocet, Hezekia Mwalugaja, amesema msaada huo ni muhimu katika kituo chao na kwamba utataweza kusaidia changamoto ya chakula.

Mwalujaga amesema Mkikita imechagua sehemu sahihi katika kutoa msaada huo wa unga kwani ni dhahiri kituo kinahitaji na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo.

“Kimsingi hamjakosea kuja Hocet kwani tunawahitaji sana watu kama nyie lakini pia katika kituo tunafundisha masomo ya kilimo hivyo tunaenda pamoja kimtazamo na kupitia nafasi hii vijana watakuwa wamemahasika,” amesema.

Kwa upande wake Hamida Shaaban, mmoja wa watoto katika kituo hicho amesema msaada huo umesababisha watambue kuwa wapo watu wanaowajali licha ya hali zao.

No comments:

Post a Comment