Sunday, 27 May 2018

Mpina ataka kupimwa na kuwekwa alama maeneo ya minada kuepuka uvamizi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye
miwani) akikagua moja ya  pikipiki 10 kabla ya kuzikabidhi ili zitumike kwenye minada ya mipakani na upili.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye
miwani) akikata utepe kwenye moja  kati ya  pikipiki 10
kabla ya kuzikabidhi ili zitumike kwenye minada ya mipakani na upili.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye
miwani) akiendesha  moja  kati ya  pikipiki 10 baada
ya kuzikabidhi ili zitumike kwenye minada ya mipakani na upili. (PICHA ZOTE NA JOHN MAPEPELE)

John Mapepele

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameagiza maeneo yote ya minada ya awali na upili yapimwe na kuwekwa alama za mipaka katika mwaka wa fedha 2018/19 ili kuepuka uvamizi unaofanywa na watumiaji wengine wa ardhi.

Maelekezo hayo ameyatoa leo kwenye hafla iliyofanyika kwenye Ofisi ya Dar es Salaam wakati akikabidhi pikipiki kumi ili zitumike kwenye mipaka na minada ya upili kwa lengo la kudhibiti utoroshaji wa mifugo na mazao yake nje ya nchi.

Amesema Serikali inakusudia kuifunga minada yote iliyoanzishwa kiholela kwa nia ovu ambapo amesema kuendelea kubaki kunadhoofisha minada ambayo imeanzishwa kwa kufuata taratibu za Serikali.

Aidha, Waziri Mpina amesema kuanzia sasa minada yote itaboreshwa na kuwa katika mfumo wa kielektroniki ili
kudhibiti mapato ya Serikali kwa njia za kisasa zaidi.

“Kuanzia sasa wizara yangu inaingia kwenye mfumo mpya katika kusimamia minada yote ambapo utaiunganisha kwenye mfumo wa kielektroniki” amesisitiza Mpina.

Sanjari na hilo Mpina amemwagiza Katibu Mkuu
anayeshughulikia Sekta ya mifugo,  Dk. Mary Mashingo kuhakikisha miundo mbinu ya minada yote inakarabatiwa mara moja na ili kuboresha usimamizi wa sekta ya mifugo nchini.

Amesema wizara inasimamia minada 12 ya upili na 10 ya mipakani ambapo ya upili ipo nchi nzima kwa kuzingatia wingi wa mifugo katika eneo husika.

Mpina amesema hapa nchini kuna minada 465 ya awali ambayo huendeshwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM).

Aidha, minada ya mipakani imewekwa kuzingatia njia za kusafirishia mifugo kwenda nje ya nchi.

Ametaja minada ya upili na wilaya ilipo kuwa ni Pugu (Ilala), Kizota (Dodoma), Sekenke (Iramba), Igunga (Igunga), Ipuli (Tabora) na Mhunze (Kishapu). Mingine ni Nyamatala (Misungwi), Meserani (Monduli), Themi (Arumeru), Weruweru (Hai), Korogwe (Korogwe) na Lumecha (Songea).

Aidha, minada ya mipakani ni pamoja na Buhigwe (Kasulu), Kasesya (Kalambo), Kileo (Mwanga), Kirumi (Butiama), Longido (Longido) na Waso (Ngorongoro).

Minada mingine ni Mpemba (Momba), Kakonko (Kakonko), Mtukula (Misenyi) na Rusumo (Ngara). Minada itakayokabidhiwa pikipiki ni Muhunze, Sekenke, Ipuli, Korogwe, Weruweru, Lumecha, Kasesya, Murusagamba, Buhigwe na Kirumi.

Ameongeza kuwa lengo la kuwepo kwa minada ya mifugo katika maeneo mbalimbali nchini ni kutoa fursa kwa wafugaji na wafanyabishara ya mifugo kuuza mifugo yao kwa faida zaidi kwa kuzingatia ushindani wa soko.

Naye katibu Mkuu Dk. Mashingo amemshukuru Waziri kwa kuzindua matumizi ya pikipiki hizo na kuahidi kwamba zitaleta ufanisi katika utendaji kazi wa minada hapa nchini.

Amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na ng’ombe millioni 30.5, mbuzi million 18.8, na kondoo millioni 5.7. Aidha, Katika mwaka 2017/18  ng’ombe 1,614,321, mbuzi 1,340,222 na kondoo 315,636 wenye thamani ya
sh. trillioni 1.1 waliuzwa katika minada mbalimbali hapa nchini.

Dk. Mashingo amesema kutokana na mifugo hiyo tani 679,962 za nyama zimezalishwa ambapo tani 1,248.4 za nyama ya mbuzi, 1,030.79 za nyama ya ng’ombe, tani 50 za nyama ya kondoo na tani 280 za nyama punda zenye thamani ya dola za Marekani billioni 5.7 ziliuzwa katika nchi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment