Saturday, 5 May 2018

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu azindua umeme katika kata za Lugoba, Madera mkoani Pwani

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati mstari wa kwanza) akiwasha rasmi umeme katika kijiji cha Hondogo kata ya Mandela, mkoani Pwani. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na wengine wanaoshuhudia ni wataalam waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliyenyanyua mkono akishangilia baada ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji cha Hondogo, kata ya Mandela na mwenye shati la kijani ni mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete. Wengine ni watumishi kutoka Wizara ya Nishati, Tanesco, Wakala wa Nishati ya Umemu Vijijini (Rea), uongozi wa halmashauri ya Chalinze pamoja na wananchi wa kata hiyo.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akielekea katika eneo la tukio la uzinduzi rasmi wa kuwasha umeme katika kijiji cha Hondogo. Kulia ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na wananchi wa kata ya Mandela.


Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akihutubia wananchi wa kata ya Mandela pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika kijiji cha Saleni kata ya Lugoba, wanaoshuhudia ni watumishi kutoka Wizara ya Nishati, Tanesco, Rea, uongozi wa halmashauri ya Chalinze na wananchi wa kata ya Lugoba.

Rhoda James, Pwani

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amezindua rasmi upatikanaji wa huduma ya umeme katika kijiji cha Saleni, Kata ya Lugoba na kijiji cha Hondogo, Kata ya Mandela mkoani Pwani.

Uzinduzi huo umefanyika Mei 3, 2018 katika vijiji hivyo wakati alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa Ujazilizi na miradi mingine ya umeme inayotekelezwa mkoani humo na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mgalu aliwaagiza watumishi wa Tanesco na Rea kuhakikisha wanaunganishia wananchi wote umeme kwa wakati ili wafaidike na nishati hiyo kwa maendeleo ya kiuchumi.

Pia aliwataka wananchi wa Pwani kuchangamkia fursa ya mradi huo pindi umeme unapofika katika kata zao.

“Fanyeni 'wiring' haraka katika zahanati na shule pia katika nyumba zenu ili muunganishiwe umeme wa Rea kwa gharama ya sh. 27,000 tu,” amesema Mgalu.

Mgalu pia amefafanua kuwa tayari kaya 65 katika kata ya Mandela zimeunganishwa umeme na nyingine 85 zimeongezwa kwa ajili ya utekelezaji.

Ameongeza kuwa ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote nchini vitakuwa vimepata umeme kwa kuwa tayari wakandarasi wote wamesha idhinishiwa malipo yao na hivyo kuwataka ambao wameondoka katika maeneo yao kurudi haraka.

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Lugoba, Rehema Issa amesema wananchi walichelewa wenyewe kufanya 'wiring' kutokana na sababu mbalimbali lakini sasa watafanya haraka.

“Pia tulikuwa na tatizo la transforma lakini sasa tumewekewa na wananchi wangu watapata umeme,”amesema Issa.

Aidha, Diwani Issa amesema yapo baadhi ya maeneo ambayo hayajapata umeme hivyo alitumia fursa hiyo kumuomba Naibu Waziri Mgalu asaidie ili vijiji vipate umeme kwa wakati.

Kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Jimbo la Chalize, Ridhiwani Kikwete alimshukuru Naibu Waziri Mgalu kwa kutembelea jimbo lake na kwa kasi kubwa ya kuhakikisha wananchi wote wa Pwani wanapata umeme kwa wakati.

No comments:

Post a Comment