Tuesday, 29 May 2018

NBS kukusanya takwimu kwa njia ya satelaiti na vishikwambi

Mrasimu ramani mwandamizi kutoka NBS, Benedict Mgambi akieleza kwa wanahabari faida za kutumia mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za kijiografia wakati wa ziara yao iliyolenga kujionea jinsi ofisi ya hiyo inavyotekeleza majukumu yake katika ukusanyaji wa taarifa mbalimbali ikiwemo sensa na tafiti zinazofanywa kwa kutumia mfumo huo wa kisasa.

Mtaalamu wa masuala ya jiografia kutoka NBS, Matha Macha  akitoa maelezo kuhusu namna mfumo huo unavyofanya kazi.

Mrasimu ramani msaidizi kutoka NBS, Rahim  Mussa akizungumzia namna mfumo huo unavyochochea maendeleo.

Mrasimu ramani mwandamizi kutoka NBS, Benedict Mgambi akiongoza ujumbe kutoka ofisi hiyo na wanahabari ambao walitembelea  kijiji cha Sasa, kujionea mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za kijiografia ikiwemo sensa na tafiti zinazofanywa kwa kutumia mfumo huo wa kisasa.

Mwenyekiti wa kijiji cha Sasa, wilaya ya Chamwino na  ujumbe wa NBS pamoja na wanahabari waliotembelea kujionea mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za kijiografia wakati wa ziara yao iliyolenga kujionea namna ofisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake ya ukusanyaji wa taarifa mbalimbali ikiwemo sense na tafiti zinazofanywa kwa kutumia mfumo huo wa kisasa. (PICHA NA FRANK MVUNGI- MAELEZO

Beatrice Lyimo- MAELEZO, Dodoma

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeanzisha mfumo wa ukusanyaji taarifa kwa kutumia teknolojia mpya na ya kisasa ya kielektroniki kwa njia ya satelaiti  na vishikwambi.

Akizungumza na wanahabari leo mkoani Dodoma, mrasimu ramani mwandamizi na msimamizi wa sehemu ya mfumo wa Ukusanyaji na Usambazaji wa taarifa za Kijiografia (GIS), Benedict Mgambi amesema lengo la mfumo huo ni kuboresha ukusanyaji wa  taarifa na tafiti mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Mgambi amesema teknolojia hiyo mpya imerahisisha kwa kiasi kikubwa ufanyaji kazi ikilinganishwa na taratibu zilizokuwa zikitumika awali.

“Awali tulikuwa tunatumia teknolojia duni ambapo mchakato wake ulihusisha watu wengi, gharama kubwa ila kwa sasa hivi kila kitu kinafanyika eneo husika la tafiti na kutumwa moja kwa moja makao makuu,” amesema Mgambi.

Aidha, Mgambi ameongeza kuwa mchakato huoumeshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo, Tamisemi, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maliasili na utalii.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Kijiografia  wa NBS, Martha Macha amesema mfumo huo umerahisisha utendaji kazi wao kwani unasaidia kutambua mipaka mbalimbali kati ya kitongoji kimoja na kingine.

“Vifaa hivi vinafanya kazi kubwa kwa muda mfupi na pia vinafanya kazi kwa ubora ule unaohitajika kwa kuona vielelezo mbalimbali vitakavyokuwezesha kufanya kazi kwa urahisi,” amefafanua Macha.

Hadi sasa vijii vitano vya Sasajila, Suli, Fufu, Champumba na Chiboli vya wilaya ya Chamwino, mkoa wa Dodoma vimefanyiwa majaribio ya mfumo huo.

No comments:

Post a Comment