Wednesday, 9 May 2018

Palole yawatoa gerezani wafungwa 63 ArushaMwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustine Mrema

Wankyo Gati, Arusha

WAFUNGWA 63 waliokuwa wanatumikia vifungo vya aina mbalimbali katika magereza mkoani hapa, wamenufaika na mpango wa Parole unaotoa nafasi kwa mfungwa kutumikia kifungo cha nje baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na bodi ya mpango huo taifa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamo kwenye taarifa fupi ya katibu wa bodi ya Parole ya mkoa wa Arusha, kamishna msaidizi mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Hamisi Nkubasi wakati wa uzinduzi wa bodi ya saba ya Parole ya mkoa iliyofanyika mkoani hapa. 

Mpango wa Parole ulianzishwa rasmi hapa nchini baada ya kupitishwa kwa sheria ya bodi ya parole  no. 25 ya mwaka 1994 na sheria yake kuanza kutumika mwaka  1999 ili kuwasaidia wafungwa wanaokidhi vigezo  kuwa karibu na familia wakiwa wanaendelea kutumikia adhabu, kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na kuipunguzia serikali gharama za uendeshaji.

Pia wafungwa wanaohusika na mpango huu kuwa ni wale wenye vifungo virefu kuanzia miaka minne na kuendelea lakini baadhi ya makosa ambayo yanagusa hisia za jamii kama vile ya unyanganyi wa kutumia silaha, ubakaji, ulawiti na mauaji hao hawatahusiki na mpango huu kutokana na aina ya makosa yao.

Kamishna msaidizi Nkubasi amesema licha ya mafanikio hayo, bado bodi hiyo inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo uhaba wa fedha na vitendea kazi katika kukusanya taarifa kwa ajili ya majalada ya wafungwa.

Na baadhi ya waathirika kuwa na elimu ndogo ya parole na hivyo kushindwa kutoa ushirikiano kwa maofisa wa parole hali ambayo inakwamisha kupata taarifa za wafungwa.

Kwa upande wake mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Mwalimu mstaafu David Marandu anatoa mwito kwa wajumbe wenzake kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria ili kufikia lengo la serikali la kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani. 

Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Arusha, Richard Kwitega amewataka wajumbe wa bodi hiyo kutokubali kuwapitisha wafungwa wasiokidhi vigezo badala yake wazingazitie maelekezo ya bodi hiyo ili kufanya uamuzi unaojitosheleza kwa maslahi ya Serikali na Taifa.

Pia amewataka wananchi kutoa ushirikinao kwa wasimamizi wa parole pindi wanapohitaji kupata taarifa sahihi za wahalifu kwa kutoa taarifa zenye ukweli bila kupotosha.

No comments:

Post a Comment