Sunday, 6 May 2018

Sirro Cup Kibiti kuzinduliwa kesho


Jeshi la Polisi
MICHUANO ya kuwania kombe la Sirro Kibiti mwaka 2018 inatarajiwa kuzinduliwa kesho Jumatatu Mei 7 na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro katika uwanja wa Samora wilayani Kibiti.
Akizungumza wilayani Kibiti baada ya kukagua maandalizi hayo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna msaidizi wa Polisi Barnabas Mwakalukwa amesema uzinduzi huo utahudhuriwa pia na viongozi mbalimbali kutoka mkoa wa Pwani.
IGP Simon Sirro

Mwakalukwa amesema lengo la michezo hiyo ni kuwaweka pamoja na kudumisha usalama kwa  wakazi wa wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji baada ya matatizo yaliyowakumba kumalizika.

Ametoa mwito kwa  wakazi wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia burudani mbalimbali pamoja na maneno ya viongozi mbalimbali yatakayotolewa katika ufunguzi wa michezo hiyo ambapo ratiba itaanza saa nne asubuhi.

Kwa upande wake Mratibu wa kombe hilo, Koplo Ramadhan Tamimu amesema michuano hiyo itakapofikia tamati bingwa atajinyakulia kombe na fedha taslimu sh. milioni moja huku ikichagizwa na kauli mbiu ya “Kibiti salama, jamii Salama”.

Naye katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu, wilaya ya Kibiti Rashid Mkinga amesema wamejiandaa vema na ana uhakika kombe hilo kubaki wilayani kwake kwa kuwa pamoja na kuwa na timu bora lakini pia wanatarajia kupata mashabiki wengi.

Ufunguzi huo utapambwa na burudani mbalimbali zikiongozwa na  Bendi ya dansi ya Jeshi la Polisi, Msanii wa nyimbo za asili Ndolela, Man Prince na vikundi mbalimbali kutoka wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

No comments:

Post a Comment