Tuesday, 1 May 2018

Stormy Daniels amshtaki Trump kuhusu ujumbe wa Twitter


Stephanie Clifford (kushoto) na Rais wa Marekani, Donald Trump.

MWIGIZAJI wa filamu za ngono Stormy Daniels amemshtaki Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu ujumbe wa Twitter anaodai ni wa kumharibia jina, wakili wake amesema.
Daniels, ambaye jina lake halisi ni Stephanie Clifford, anasema alitishiwa na mwanamume mmoja katika maegesho ya magari mjini Las Vegas na kutakiwa kuacha kuendelea na madai yake kwamba aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Trump.
Rais huyo wa Marekani alipakia kwenye Twitter mchoro wa mwanamume mshukiwa na kisha kuandika "hii ni kazi ya utapeli kabisa".
Wakili wa Daniel aliandika kwenye Twitter kwamba Trump "anafahamu vema kabisa yaliyotokea".

"Trump alitumia fursa ya mamilioni ya watu katika taifa hili na kimataifa (wanaomfuatilia katika mtandao huo wa kijamii) kutoa taarifa ya uongo yenye lengo la kumshushia hadhi na kumshambulia Clifford," kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya dola mjini New York inasema.

Kesi hiyo inasema ujumbe huo wa rais ulikuwa wa kumharibia mtu jina kwani ulimtuhumu Daniels kwa "kutekeleza kosa kubwa" - hususan, la kumtuhumu mtu mwingine kwamba alimtishia.
Trump alikuwa amepakia mtandaoni mapema mwezi huu picha ya mchoro wa mshukiwa huyo na kumweleza kuwa "mwanamume asiyekuwepo".
Daniels anasema yeye na rais huyo walikuwa na uhusiano wa kimapenzi kuanzia 2006. Trump amekanusha tuhuma hizo.
Mwanamke huyo aliambia kipindi cha CBS News kwamba baada ya kutamatika kwa uhusiano wao, mwanamume mmoja alifika alipokuwa yeye na binti yake katika maegesho hayo ya magari Las Vegas na kumwambia "sahau taarifa hiyo, mwache Donald Trump".
Daniels awali alimshtaki wakili wa Trump, Michael Cohen, akitaka kuvunjwa kwa mkataba wa kutofichua siri kuhusu uhusiano huo, ambao anasema Trump hakuutia saini.
Cohen awali alikiri kwamba alimpa Daniels $130,000 zake mwenyewe, lakini alisema kwamba hakueleza ni kwa nini alitoa fedha hizo.
Kesi hiyo hata hivyo ilisitishwa kwa siku 90, huku jaji akisema kwamba haki za Cohen zingekuwa hatarini iwapo kesi hiyo ingeendelea akiwa bado anachunguzwa.
Cohen anachunguzwa na Mwanamashtaka maalum Robert Mueller kuhusu tuhuma kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 na kwamba taifa hilo lilishirikiana na maofisa wa kampeni wa Rais Trump.
BBC

No comments:

Post a Comment