Friday, 4 May 2018

TFCG, Mjumita wawafunda maofisa maliasili, mazingira


Meneja Mradi wa Kuleta Mabadiliko katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), Charles Leonard akitoa mafunzo kwa maofisa wa serikali kutoka sekta ya maliasili, misitu, mazingira na mipango kutoka wilaya 10 kuhusu mkaa endelevu. PICHA NA SULEIMAN MSUYA)

Mwandishi Wetu, Morogoro

MAOFISA maliasili, misitu, mazingira na mipango zaidi ya 40 kutoka wilaya mbalimbali wametakiwa kusimamia misitu ya vijiji ili iwe endelevu.

Hayo yamesemwa na Ofisa Maliasili Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa wakati akifungua mkutano wa maofisa hao uliondaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita).

Maofisa hao zaidi ya 40 wametokea katika wilaya za Kilosa, Morogoro, Mvomero, Handeni, Kilindi, Kilwa, Tabora, Uvinza, Kigoma na Kilolo.

Chuwa amesema katika kukabiliana na uharibifu wa misitu kwenye vijiji maofisa misitu, maliasili, mazingira na mipango miji wanapaswa kushirikiana na wananchi kwa ukaribu.

"Misitu mingi nchini ipo katika usimamizi wa vijiji huku serikali kuu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), ikisimamia eneo dogo hivyo ni imani yangu mkitoka hapa mtakuwa mabalozi wazuri katika kusimamia sekta hii muhimu," amesema.

Chuwa amesema katika kuhakikisha dhana ya utunzaji misitu inaonekana kwa vitendo ni lazima wasimamizi kujitoa kwa maslahi ya nchi.

Amesema mkoa wa Morogoro umefanikiwa kutunza misitu asili kwenye vijiji 30 vya wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro vijijini.

Amesema asilimia kubwa ya watanzania hasa maskini wanatumia rasilimali za misitu katika mahitaji ya kila siku hivyo bila kushirikiana nao ni vigumu kulinda misitu.

Kwa upande wake mtoa mada Meneja Mradi wa Kuleta Mabadiliko katika Sekta ya Mkaa  (TTCS), Charles Leonard amesema katika kukabiliana na uharibifu wa misitu nchini wamekuja na mradi huo hasa kwa misitu ya miombo.

Amesema asilimia 90 ya misitu nchini ni miombo ambayo zaidi ya asilimia 40 ipo katika ardhi za vijiji hivyo wamekuwa wakiwashirikisha serikali na wanavijiji kuitumia kiendelevu.

Meneja huyo amesema katika kuendeleza misitu hiyo kwa shughuli za kijamii wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya jinsi ya kuvuna na kuwa endelevu kwa muda mrefu.

"Miombo ni asilimia 90 ya misitu nchini hivyo tumejikita katika misitu hii ili kukata mkaa endelevu bila kuathiri misitu iliyopo," amesema.

Ameongeza kuwa mradi huo unafanya ufuatiliaji wa miti inayovunwa ambapo zaidi ya asilimia 70 miti iliyokatwa imechipua ikiwa ni pamoja na mbegu zilizofunikwa kuanza kuota.

Leonard amewaambia maofisa hao kuwa ufanisi wa mradi umepatikana kutokana na kuwapatia elimu wanakijiji kupitia kamati ya maliasili ya kijiji.

No comments:

Post a Comment