Wednesday, 2 May 2018

Ubovu wa barabara Kilolo Kabati amwangukia MagufuliRita Kabati
Claudia Kayombo

MBUNGE wa Viti Maalum mkoa wa Iringa, Rita Kabati (CCM), amemwomba Rais Dk. John Magufuli kutengeneza barabara nyingi za wilaya ya Kilolo kwa kuwa hazipitiki kutokana na jiografia ya wilaya hiyo.

Kabati amesema ubovu wa miundombinu ya barabara unachangia kinamama wengi hususan wajawazito kukumbwa na changamoto kubwa ya kuzifikia huduma za afya.

Ametoa ombi hilo leo, Mei 2, 2018, wilayani Kilolo ambapo alikuwa mmoja wa wabunge wa mkoa wa Iringa ambao walipewa nafasi ya kusalimia wananchi mara baada ya Rais Dk Magufuli kufungua hospitali ya Kilolo.

Amesema jiografia ya wilaya ya Kilolo baadhi watu wanaishi mabondeni wengine milimani huku barabara nyingi zikihitaji matengenezo ili waweze kufika kwa urahisi maeneo ya kutolea huduma mbalimbali zikiwemo za afya.

Pia amemwomba Rais kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya wanapelekwa katika hospitali hiyo na nyingine ambazo zinakabiliwa na tatizo la wataalam wa afya sanjari na dawa za usingizi kwa wagonjwa.

“Mheshimiwa Rais licha ya kuwa tumekatazwa kuzungumza mengi kwa kuwa hadhara hii si yetu, nikuombe tu mambo machache, jiografia ya Kilolo wapo watu wanaoishi milimani na wengine mabondeni, hali ya barabara nayo si nzuri, kinamama wengi wanapata tabu sana wanapofuata huduma za afya hivyo nikuombe tutengenezee barabara hizi.

“Pia ujenzi wa hospitali unapokamilika tunaomba wataalamu, tuna uhaba wa dawa za usingizi na gari la kubebea wagonjwa lipo moja tu, hivyo tunaomba jingine,” amesema Kabati.

Wakati wa hotuba yake Rais Dk. Magufuli ameahidi kuwaleta wahudumu wa afya wa kutosha katika hospitali hiyo na kuahidi kujenga baadhi ya barabara za wilaya hiyo na nyingine za mkoa mzima wa Iringa.

No comments:

Post a Comment