Tuesday, 29 May 2018

Ujenzi kituo cha ukaguzi Manyoni kukamilika Septemba


Mhandisi mkazi wa Kampuni ya Kizalendo ya NIMEA Consult (T) ltd, Eng. Patrick Lutinya akimwonesha naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (wa kwanza kushoto) hatua mbalimbali zilizofikiwa za ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja, kinachojengwa Manyoni, Singida, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wake. Wa tatu kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), mkoa wa Singida, Mhandisi Leonard Kapongo.Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa mhandisi mkazi kutoka Kampuni ya Kizalendo ya NIMEA Consult (T) ltd, Mhandisi Patrick Lutinya mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja, kinachojengwa Manyoni, Singida.


Tinga tinga likiendelea kushindilia matabaka mbalimbali ya barabara katika ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja, kinachojengwa Manyoni, Singida.


Muonekano wa nyumba watakazoishi watumishi mbalimbali watakaokuwa wakifanya kazi katika kituo cha ukaguzi wa pamoja, kinachojengwa Manyoni, Singida. Ujenzi wa kituo hicho kwa sasa umefikia asilimia 45 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya jengo la kituo cha ukaguzi wa pamoja. Ujenzi wa kituo hicho kwa sasa umefikia asilimia 45 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.


Mwandishi Wetu


NAIBU  Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja unaoendeshwa na Kampuni ya Impresa di Costruczioni Ing. E. Mantovan S.p.a con socio unico Via Belgio ya nchini Italia.

Amesema kukamilika kwa ujenzi huo unaofanyika wilayani Manyoni, mkoa wa Singida kutarahisisha uchukuzi katika nchi za ukanda wa kati.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Kwandika amesema ni utekelezaji wa maazimio ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kupunguza ucheleweshaji wa huduma za uchukuzi kwa njia ya barabara hususan wa mizigo inayoelekea nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

“Niwapongeze kwa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi huu kwani kukamilika kwake, kutapunguza muda unaopotezwa na madereva wanaosafirisha mizigo nje ya nchi baada ya sasa kuwa wanakaguliwa kwenye vituo zaidi ya 30 nchini,” amesema Kwandikwa.

Aidha, amewataka wananchi wa wilaya ya Manyoni kutumia fursa ya uwepo wa kituo hicho kuanza kujenga sehemu za huduma ya chakula ili  kupitia uwekezaji huo wapate kipato na kuinua uchumi wao.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Singida, mhansisi Leonard Kapongo, amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa atamsimamia  mkandarasi huyo na kuhakikisha kasi inaendana na viwango vilivyopo kwenye mkataba ili mradi ukamilike kwa wakati.

No comments:

Post a Comment