Friday, 4 May 2018

Wakulima nchini kuunganishwa na masoko ya Ulaya

Sulemain Msuya

MTANDAO wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita), unatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku saba katika nchi nne za Bara la Ulaya ili kuunganisha wakulima na masoko, teknolojia, mitaji, uwekezaji na kujenga ushirikiano wa kibiashara.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mkikita, Adam Ngamange katika mahojiano maalum.

Ngamange amesema ziara hiyo ambayo itaanza Mei 7 hadi 18 mwaka huu itahusisha  nchi ya Italia, Uturuki, Uswis na Uholanzi ambazo zimekuwa na uhitaji wa bidhaa za Tanzania.

 Adam Ngamange

Amesema safari hiyo ambayo wameiita ya  maono inalenga kuwakilisha wakulima na watanzania katika kutafuta masoko ya mazao na bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.

"Mkikita kupitia mimi tumeandaa safari ambayo tumeiita safari ya maono katika nchi nne za Ulaya yaani Uturuki, Uswis, Italy na Uholanzi kutangaza mazao na bidhaa zetu.

“Hii ni ziara ya kipekee kwa Mkikita kutembelea nchi hizo kwa mualiko wa Kampuni ya MPA (Uturuki), LoccoZ (Uswis na Uholanzi)  na ITA-Italian Trade agents (Italia)," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema pia safari hiyo imelenga kutangaza na kuunganisha Mkikita kwa ajili ya wanachama na watanzania kwenye eneo la masoko, teknolojia na mitaji ya uwekezaji 

Amesema matarajio yao  ni kupata fursa ya masoko makubwa ya mbogamboga, mihogo, viazi lishe, matunda na viungo. 

"Imani yetu ni ziara hiyo tutapata wawekezaji na marafiki wa biashara katika sekta ya kilimo lakini pia kufungua milango mikubwa ya teknolojia ya kilimo biashara," amesema.

Ngamange amesema  fursa hiyo siyo yake  wala Wanamkikita ni kwa nchi nzima na kuwataka watanzania kuitumia.

Aidha, Ngamange amewaomba watanzania kujitokeza kushiriki kilimo biashara ambacho kinafanywa na Mkikita hasa eneo la Kiwangwa wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment