Monday, 28 May 2018

Wakulima Pwani wahimizwa kulima pamba kujikwamua kiuchumi

Shamba la pamba lililopo Kweikonje ,Chalinze Bagamoyo mkoani Pwani ambalo limestawi na kuendelea vizuri.

Ofisa kilimo na ushirika wa halmshauri ya Chalinze, Jovin Bararata akiangalia namna pamba inavyostawi katika moja ya shamba la mkulima wa zao hilo eneo la Kweikonje, Bagamoyo.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo alipotembelea shamba la pamba la Rashid Msilu huko Chalinze, Bagamoyo ambapo alihimiza wakulima kulima zao hilo. (PICHA NA MWAMVUA MWINYI)

Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

WAKULIMA wa mazao ya biashara mkoani Pwani, wamehamasishwa kulima kilimo cha pamba ili kujiinua kiuchumi.

Mkuu wa mkoa huo, mhandisi Evarist Ndikilo amehimiza kilimo hicho, wakati alipokwenda kutembelea shamba la pamba la Rashid Msilu lililoko eneo la Kweikonje, Bagamoyo.

Aidha, amekemea utoaji wa dawa za viuadudu vinavyoshambulia zao hilo ambazo ni feki na kudai mtu atakayekamatwa anazigawa atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani anasababisha kudididimiza juhudi za wakulima hao.

Amesema katika mkoa huo maeneo yanayostawi zaidi kilimo cha pamba ni wilaya ya Rufiji na Chalinze.

Ndikilo amebainisha kuwa kipindi cha nyuma kilimo hicho kilitetereka lakini sasa mazingira na ardhi inaruhusu kukiinua.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, kupitia wizara ya kilimo imeshasambaza mbegu bora ya pamba, mabomba ya kupulizia dawa kwa mkopo na dawa za viuadudu zimetolewa bure.

Ndikilo amefafanuakuwa, Chalinze imeshapatiwa lita 226 za dawa ya kupulizia kuzuia wadudu waharibifu ambapo Rufiji imepewa lita 120 na mabomba ya kupulizia dawa  lita nyingine 40 kwa ajili ya Chalinze.

Ameomba dawa hizo ziwafikie wakulima wa pamba ili kuleta tija.

“Kuhusu dawa feki nimesikia kwa baadhi ya wakulima kuwa mwaka jana zililetwa, hazikuua wadudu, kwakweli kipindi hiki sitokubali kusikia tatizo hilo tena” amesisitiza Ndikilo.

Pamoja na hayo, amekemea pasiwepo na hujuma wakati wa hatua ya uvunaji .

“Kuna baadhi ya wakulima wanaweka maji ,mawe ,mchanga kwa lengo la kuongeza uzito, msifanye hivyo mnashusha sifa ya mkoa na Taifa,"Ndikilo amesema.

Pia vyama vya msingi viwe na maghala, mizani halali na vifungashio bora ili kupeleka vyama vya ushirika kupata masoko ya uhakika.

Amelezea mwaka jana alisikia chama cha ushirika -Corecu hakikuchukua pamba za wakulima kutokana na kukosa fedha, hivyo aliwahakikishia wakulima ataongea na mwenyekiti wa Corecu kuangalia namna ya kununua pamba hiyo.

Naye ofisa kilimo, umwagiliaji na ushirika, Chalinze Jovin Bararata amesema halmashauri ya Chalinze ni moja ya halmshauri zinazolima pamba mkoani humo.

Amebainisha kuwa mwaka jana walivuna tani 63 na mavuno yajayo wanatarajia kuvuna tani 250.

Bararata ameelezea kuwa wamejiwekea mikakati ya kuhamasisha kilimo hicho ambapo wamenunua pikipiki 15 ambazo watagawiwa maofisa ugani ili waweze kuwatembelea wakulima mbalimbali kirahisi.

Mkakati mwingine ni kukabiliana na tatizo la soko kwa kuimarisha vyama vya msingi ili kuhakikisha vinaratibu vizuri na kukusanya pamba”:, wakulima waweze kunufaika na mfumo wa stakabadhi ghalani.

Bararata amesema ipo changamoto ya wadudu waharibifu na panya ambapo wanadhibiti hali hiyo kwa kushirikiana na bodi ya pamba kwa kuhakikisha dawa zinagawiwa kwa wakati.

Mkulima wa pamba Mzee Rashid Msilu ameishukuru serikali kwa kuwapatia dawa, mbegu bora ili kulima kisasa.

Nchi ya Tanzania inaingiza fedha nyingi za kigeni kwa mazao ya biashara makubwa matano ikiwemo kahawa, chai, korosho, pamba na tumbaku lakini zao linaloongoza ni korosho.

Kwa mkoa wa Pwani, zao la biashara linaloingiza fedha za kigeni ni korosho ambapo kwasasa serikali mkoani humo inahimiza pamba ili kuwa na mazao mawili ya kibiashara.

No comments:

Post a Comment