Thursday, 17 May 2018

Wakuu wa mikoa Kanda ya Ziwa wakosoa wanasiasa wanaoipaka matope serikali kuhusu dhamira yake ya kupambana na uvuvi haramu

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akihutubia hadhara ya kikosi kazi cha watu 260 (hawapo pichani) alichokiunda kwa ajili ya operesheni Sangara 2018 na wakuu wa mikoa mitano inayozunguka Ziwa victoria wakati wa mkutano wa kufanya tathmini ya operesheni  hiyo.


Viongozi wakuu wa Wizara  ya  Mifugo na Uvuvi waliokaa  wakiwa katika picha ya pamoja na makamanda wakuu wa Operesheni Sangara 2018 (waliosimama) wakati wa mkutano wa kufanya tathmini ya operesheni  hiyo. 

Viongozi wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliokaa wakiwa katika

picha ya pamoja na sekretarieti ya Operesheni Sangara 2018 (waliosimama)
wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo. (PICHA ZOTE NA JOHN MPELE


John Mapepele, Mwanza

WAKUU wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria wamekosoa tabia ya

baadhi ya wanasiasa kuipaka matope dhamira njema ya Serikali ya
kupambana na uvuvi haramu ulioshamiri katika ziwa hilo.


Wamewataka viongozi hao kutangaza maslahi yao kwenye eneo la uvuvi kabla ya kuwashambulia viongozi wanaosimamia mchakato huo kwa misingi ya kisheria.

Wakizungumza kwenye kikao cha tathmini ya operesheni sangara awamu ya

pili iliyowahusisha wakuu wa mikoa, wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, makamanda wa Polisi wa mikoa na wakuu wa idara ya usalama wa taifa wa mikoa yote inayozunguka Ziwa Victoria jijini Mwanza jana viongozi hao wametaka hatua zaidi zichukuliwe ili kunusuru rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.


Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka ameonesha wazi kuchukizwa na tabia inayoanza kuota mizizi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuipaka matope dhamira nzuri ya Serikali ya kukabiliana na uvuvi haramu na kutaka

viongozi wa aina hiyo watangaze masilahi yao kabla ya kuanza
kuwashambulia viongozi wanaosimamia operesheni hiyo inayotekelezwa kwa mujibu wa sheria.


“Viongozi wanaopinga operesheni ya kupambana na uvuvi haramu ni muhimu watangaze kwanza masilahi yao kuhusu eneo la uvuvi ili wasiendelee kuchafua taswira za viongozi wanaosimamia wizara hii,” amesema Mtaka.

Naye mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela amesema kumekuwepo na dhana zinazojengeka kwamba viongozi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria hawaungi mkono mapambano ya kukabiliana na uvuvi haramu jambo ambalo ni upotoshaji mkubwa na kwamba serikali ya mkoa wake  iko mstari wa mbele kuwabana watendaji wa ngazi zote watakaobanika

kufadhili uvuvi haramu.


Amesema ni muhimu operesheni hiyo iwe endelevu na kubainisha kuwa suala la uvuvi haramu haliwezi kumalizika kama hakuna dhamira ya dhati

miongoni mwa wasimamizi wa sheria na kwamba uongozi wa mkoa huo
hautakubali kuendelea kuwa na watumishi wazembe wataoshindwa kusimamia suala hilo.


Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametangaza

kuanza Awamu ya Tatu ya Operesheni Sangara yenye lengo la kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria sanjari na kutangaza operesheni katika maziwa yote na kuagiza viongozi wakuu wa mikoa na wilaya kuwachukulia hatua kali viongozi wa chini wanaobanika kujihusisha na kufadhili uvuvi haramu.


Pia ametangaza kuunda kanda mpya ya udhibiti na usimamizi rasilimali za

uvuvi katika wilaya za Ukerewe na Sengerema huku akiunda ofisi mpya ya
Kanda jijini Mwanza itakayokuwa inaratibu shughuli zote katika kanda
hizo ili kuongeza usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo.


Aidha, Mpina ameongeza kuwa katika awamu ya tatu ya operesheni hiyo

itahusisha pia mahakama zinazotembea ili kuweza kutoa hukumu huko huko ziwani hali itayowezesha kuondokana na uvuvi haramu.


Aidha, amewataka watu wote wanaopinga operesheni ya uvuvi haramu wasome takwimu ili kujua ukubwa wa tatizo katika Ziwa Victoria ambapo watuhumiwa 3,284 wamekamatwa wakijihusisha na uvuvi haramu huku samaki wasioruhusiwa kilo 326,751 , mabondo kilo 5,142 zilikamatwa zikitoroshwa kwenda nje ya nchi na nyavu haramu 566,497 nazo zilikamatwa na kuteketezwa.

Pia magari 257, mitumbwi 1278 , pikipiki 269 na injini za mitumbwi 564 vilikamatwa vikihusishwa na makosa ya uvuvi haramu.


Amesema katika baadhi ya maeneo ya Bushengere wilayani Ukerewe wazazi

wamewaonya watoto wao kutotumika na mafisadi kwenye uvuvi haramu kwani wakikamatwa wao ndio wanaopata tabu na kutelekezwa ambapo wameweka azimio la kukataa kutumika tena kwenye jambo hilo.


Amesema kutokana na operesheni hizo zinazoendelea za kupambana na uvuvi haramu hadi kufikia Desemba mwaka huu watu wote wanaopinga na hata kuwaombea mabaya viongozi wa operesheni watapata aibu kubwa kwani idadi ya samaki itaongezeka huku akitoa mwito kwa viongozi wa ngazi zote wenye mapenzi mema na nchi kuunga mkono vita hiyo kwa manufaa ya Taifa.


Katibu mkuu Uvuvi, Dk. Yohana Budeba amesema wizara hiyo imejipanga

kikamilifu kuhakikisha sekta ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika pato
la Taifa na kwamba operesheni hiyo itaendelea hadi pale uvuvi haramu
utakapokoma.


Mkuu wa wilaya ya Busega, Tano Mwera amesema wamekuwa wakipokea

malalamiko mengi kuhusu operesheni hiyo lakini kila walipofuatilia
kupata ushahidi  walikosa jambo ambalo wamebaini kuwa ni njama za makusudi za kutaka kuhujumu nia njema ya Serikali ya kupambana na kutokomeza uvuvi haramu.


Kamanda Mkuu wa operesheni hiyo kutoka Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hassan Shelukindo amesema katika operesheni hiyo, watuhumiwa 22 wakiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji na viongozi wa BMU wamefungwa jela huku wengine 17 mashauri yao yakiwa yanaendelea mahakamani  kwa makosa ya kujihusisha na uvuvi haramu.

Shelukindo amesema pia watumishi 6 waliokuwa kwenye oparesheni hiyo
waliondolewa kwa makosa mbalimbali ikiwemo ukiukwaji wa maadili ya kazi ambapo watachukuliwa hatua za kinidhamu na taasisi zao huku sh. bilioni 7.5 zikikusanywa kutokana na faini pamoja mauzo ya mabondo, samaki na kayabo.

No comments:

Post a Comment