Wednesday, 2 May 2018

Wanafunzi sita Kenya watumbukia chooniVyoo vya namna hii mara nyingi hutumiwa zaidi maeneo ya vijijini


WANAFUNZI sita wa shule moja eneo la mashinani Kenay wameanguka katika shimo la choo baada ya choo hicho kuporomoka leo Jumatano asubuhi, vyombo vya habari nchini humo vinaripoti.
Leo ni siku ya kwanza ya muhula mpya katika shule ya msingi ya Kisulisuli kaika kaunti ya Nakuru mkoa wa Bonde la ufa.
Taarifa zilisambaa yapata saa mbili asubuhi kuwa choo katika shule hiyo kimeporomoka na wanafunzi wamezikwa ndani.
Wazazi walikimbia katika shule hiyo kwa haraka na mara moja jitihada za uokozi zilianza kwa ushirikiano wa jamii na maofisa wa uokozi.
Udongo mbichi ulifukuliwa na mawe yakavunjwa kuwafikiwa na kuwaokoa wanafunzi hao sita.
Awali idadi ya waliozama haikujulikana, lakini baada ya mwalimu mkuu kuwahesabu wanafunzi wote, alithibitisha kupitia vyombo vya habari nchini humo kwamba wote wako salama.
Choo hicho cha nje katika shule ya msingi ya Kisulisuli kiliporomoka baada ya mvua kubwa na mafuriko ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini humo kwa wiki nne sasa.
Uwanja wa michezo wa shule hiyo pia umefurika.
Mkasa wa leo unafuatia msururu wa mikasa kama hiyo nchini Afrika Kusini ambapo idara ya elimu sasa imetenga mpango maalum unaopiga marufuku vyoo vya mashimo katika shule za msingi.
Kituo kimoja cha televisheni kimemnukuu mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Kisulisuli aliyesema kuwa kati ya wanafunzi sita waliokolewa, wanne wako salama, lakini wawili walijeruhiwa.

BBC

No comments:

Post a Comment