Tuesday, 8 May 2018

Wananchi wana matarajio makubwa nanyi fanyeni kazi kwa kiwango cha juu - Jaji mkuu

Mary Gwera
JAJI Mkuu Profesa Ibrahim Juma amewataka majaji wapya wa Mahakama Kuu kufanya kazi kwa kiwango cha juu kwani wananchi wana matarajio makubwa na matokeo ya kazi zao.
Amesema hayo mapema Mei 07 alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika kituo cha mafunzo kilichopo mahakama  ya hakimu mkazi Kisutu-Dar es Salaam.

Jaji mkuu Profesa Ibrahim Juma

“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka, wakati ambao Mahakama ya Tanzania ipo katika maboresho mbalimbali, hivyo ni vema ninyi majaji kupitia utendaji kazi wenu mtumike kubadili taswira ya mahakama,” amesema Jaji Ibrahim.

Jaji mkuu amesema lengo la mafunzo hayo kwa majaji wapya wa mahakama kuu ni kuwapa miongozo na taratibu mbalimbali katika ufanyaji kazi ya ujaji.

“Mafunzo haya enedelevu yanayotolewa na mahakama kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni muhimu katika utendaji kazi kwani baadhi ya majaji walioteuliwa wametoka sehemu mbalimbali hivyo ni vema kuwafunza ili kuwa na uelewa wa pamoja katika utendaji kazi,” amefafanua.

Jaji mkuu pia amewataka majaji kufanya kazi kwa kuangalia pia dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.

Mafunzo hayo yamewashirikisha majaji wapya 14, 12 kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania na wawili kutoka Mahakama Kuu-Zanzibar yanafanyika kwa muda ya wiki tatu, na katika mafunzo hayo mada mbalimbali zitatolewa ikiwa ni pamoja na Matumizi ya Tehama mahakamani na makosa ya mtandao.

No comments:

Post a Comment