Sunday, 6 May 2018

Watano wahofiwa kufa maji kisiwa cha Mafia
Top of FormWATU watano wanahofiwa kufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka baharini, karibu na Kisiwa cha Mafia.
Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo juzi Ijumaa baada ya kuwepo dhoruba kali baharini.
Miongoni mwa watu watano waliofariki dunia mmoja ana asili ya Marekani wengine ni Watanzania.
Walikuwa wakisafiri kutoka bandari ya Nyamisati iliyoko wilaya ya Kibiti mkoa wa Pwani, kwenda pwani ya Kilindoni iliyoko katika wilaya ya Mafia katika shughuli za kimishionari.
Dau amefafanua kuwa walipofika katikati ya Mafia na Nyamisati kulitokea dhoruba na kusababisha chombo chao kupinduka abiria wote sita wakatumbukia baharini na kusambaratika.
Nahodha wa chombo hicho ndiye pekee aliyenusurika baada ya kuongelea hadi kijiji jirani kilichopo wilaya ya Mkuranga kwenye kisiwa cha Koma.
Manusura huyo alipatiwa huduma ya kwanza katika zahanati ya Koma na kisha baadaye kuhamishiwa katika hospitali ya Kimishionari ya Kisiju na baadaye jana alihamishimishiwa hospitali ya Agakhan, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Dau amesema wenzake watano waliokuwa wameabiri chombo hicho akiwemo raia huyo wa Marekani aliyetambuliwa kwa jina moja Kenneth, haijulikani walipo.
Juhudi za kuwasaka zinaendelea tangu juzi huku boti mbili za hifadhi ya bahari za kisiwa cha Mafia, zikitokea kisiwani humo zilitia nanga Kisiju na kumchukua nahodha aliyenusurika kumpeleka bandari ya Kisiju.
Jana boti hizo zilisaidiana na helikopta ya Jeshi la Polisi kutafuta miili hiyo kwa matumaini kuwa labda ingekutwa inaelekea baharini bila mafanikio na mchakato huo unaendelea leo katika Kisiwa cha Koma na Kwale eneo la Kisiju.
Kutokana na uzoefu wa nyakati za hali ya hewa, wakati huu ni wa msimu wa pepo za Kusi hivyo maiti hizo huenda zikaonekana Dar es Salaam ama Zanzibar, bandari za Kuruti, Kisiju, bandari ya Buza na kisiwa cha Sukuti na maeneo yote yenye mikoko ndiyo yanayotiliwa zaidi mkazo katika juhudi za kutafuta miili ya watu hao.

No comments:

Post a Comment