Friday, 11 May 2018

Watu 40 wafariki baada ya bwawa kuvunja kuta Nakuru KenyaZAIDI ya watu 40 wamefariki dunia na maelfu wengine wameachwa bila ya makazi wakati bwawa moja mjini Nakuru nchini Kenya lilipovunja kuta zake Jumatano usiku.
Shirika la kupambana na majanga nchini Kenya linasema watu wengine wengi hawajulikani waliko hadi sasa.
Eneo hilo la Solai katika kaunti ya Nakuru Kenya, lina mabwawa saba yanayotumika katika kilimo cha umwagiliaji.
Waziri wa mambo ya ndani wan chi hiyo, Fred Matiang'i amesema serikali imeanzisha uchunguzi kubaini uthabiti wa mabwawa mengine sita yaliyosalia.
Maofisa wa uokoaji kutoka mashirika tofauti nchini humo wamekuwa katika jitihada za kutafuta miili ya watu waliokufa kutokana na mkasa huo.
Mapema leo Ijumaa kulikuwa na hisia ya wasiwasi wakati taarifa zilisambaa katika mitandao ya kijamii kwamba bwawa la pili limepasuka katika eneo hilo hilo.
Msemaji katika wizara ya mambo ya ndani, Mwenda Njoka hata hivyo amekanusha taarifa hizo katika ujumbe aliotuma kwenye Twitter akieleza kwamba maji hayo yametokana na shughuli za wahandisi wanaopunguza kiwango cha maji yaliojaa katika mabwawa mengine katika kenye eneo hilo.
Njoka amesema hatua hiyo imefanywa chini ya udhibiti wa wataalamu ili kuruhusu ukaguzi wa mabwawa hayo.
Bwawa la Patel mjini Nakuru katika mkoa wa Bonde la ufa lilivunja kuta zake Jumatano usiku na kusomba mamia ya nyumba za wakazi waliokuwa karibu na eneo hilo.
Walioshuhudia wanasema walisikia mshindo mkubwa kabla ya mawimbi makubwa kuyasomba makazi na mashamba ya watu yenye umbali wa takriban kilomita mbili, eneo ambalo watu wengi wanaishi na kufanya kazi.

Jitihada za kuwatafuta manusuru zilisitishwa jana usiku kutokana na kutanda giza, hata hivyo inahofiwa kwamba huenda idadi ya watu waliofariki ikaongezeka wakati jitihada zikiendelea leo kuwatafuta manusura.
Huu ni mkasa wa kwanza wenye ukubwa wa aina hii kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya.
Zaidi ya watu 2000 wameachwa bila ya makazi. Bwawa hilo la Patel ni mojawapo ya mabwawa matatu yanayomilikiwa na mkulima mmoja mkubwa katika eneo hilo.
Inaarifiwa kwamba kuta zake zilibomoka kutokana na maji mengi yaliokusanyika kufutia mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini humo.
Viongozi wa eneo hilo sasa wanataka kujua iwapo mkulima huyo ana kibali kilichomruhusu kujenga mabwawa hayo, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hali ya mabwawa mawili yaliosalia ambayo pia yanatajwa kuwa yamejaa.

No comments:

Post a Comment