Sunday, 10 June 2018

'Flyover' ya Tazara kufunguliwa Septemba

Profesa Makame Mbarawa

Suleiman Msuya

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema daraja la Tazara ‘Flyover’ linatarajiwa kufunguliwa rasmi  Septemba mwaka huu na Rais John Magufuli.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo la kisasa.

Amesema daraja hilo ambalo linapaswa kujengwa kwa miezi 36 linataanza kutumika rasmi Septemba ikiwa ni muda sahihi kulingana na mkataba.

Waziri amesema hadi sasa  ujenzi umefikia asilimia 88.82 hivyo kama hakutakuwa na mabadiliko Septemba mwaka huu, Rais Magufuli atafungua rasmi na kuanza kutumika.

Amesema hadi kukamilika kwa daraja hilo zaidi ya sh. bil 95 zitakuwa zimetumika ikiwa ni fedha kutoka nchini Japani kupitia Shirika la Maendeleo la Japani (Jica).

“Daraja hilo la Tazara ‘Flyover’ linatarajiwa kufunguliwa rasmi Septemba mwaka huu kwani hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 88.82 na Rais ndiye anatarajiwa kulifungua,” amesema Mbarawa.
Ameongeza kuwa Agosti mwaka huu wataanza kufanya majaribio ya daraja hilo baada ya kazi zote muhimu kukamilika kama inavyotarajiwa.

Waziri Mbarawa amesema hadi sasa mkandarasi Sumotomo Mitsui Construction Co, Ltd ametumia saa milioni 2.16 ambapo ujenzi umebakia katika maeneo ya kuingilia.

Amefafanua kuwa hadi sasa hakuna ajali ambayo imetokea tangu ujenzi uanze jambo ambalo ni la kupongezwa na kwamba ni moja ya sababu ya mradi kwenda kwa kasi.

Mbarawa amesema kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza msongomano na foleni katika eneo hilo la Tazara ambapo wasafiri watatumia dakika zisizozidi 30 kutoka mjini hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

“Kwa sasa ili kufika mjini kwa kutumia barabara ya Nyerere ni zaidi ya saa mbili, ila kukamilika kwa mradi huu haitazidi nusu saa,” amesema.

Mbarawa ametanabaisha kuwa serikali kupitia wizara yake inajipanga kujenga madaraja mengine eneo la Chang’ombe, Kurasini, Mwenge, Ubungo ‘Interchange’ na Salender lengo likiwa ni mkakati wa kupunguza msongamano na foleni jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake balozi wa Japani hapa nchini, Masaharu Yoshida amesema anajisikia furaha kuona mradi huo unakwenda kwa kasi ambayo ilitarajiwa hali ambayo itapunguza msongamano wa mgari katika eneo hilo.

Yoshida amesema serikali ya Japani imedhamiria kuisaidia Tanzania katika miradi ya maendeleo kwa maslahi ya nchi.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Julius Ndyamukama, amesema changamoto zilizojitokeza katika ujenzi wa daraja hilo ni uongozaji wa magari lakini walifanikiwa kuzikabili.

Ujenzi wa daraja la Tazara lilikuwa pendekezo la Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete katika ahadi zake ambapo mkataba wa ujenzi ulisainiwa Septemba 2015.

No comments:

Post a Comment