Saturday, 9 June 2018

Jeshi la wanamaji Kenya lawatia mbaroni Watanzania 109


JESHI la wanamaji wa Kenya limewatia nguvuni watanzania 109 likiwashuku kushiriki uvuvi haramu katika himaya ya maji ya taifa hilo eneo la Bahari ya Hindi.
Wavuvi hao wamekamatwa eneo la Shimoni, linalomiliki na Bandari Kusini mashariki mwa Kenya karibu na mpaka na taifa hilo na Tanzania.
Waliwasilishwa mbele ya mahakama ya kaunti ya Kwale siku ya Jumatatu.
Wanazuiliwa baada ya kushindwa kulipa dhamana ya shilingi 20,000 za Kenya kila mmoja wao lilisema gazeti la Biashara nchini Kenya Business Daily , likimnukuu naibu wa kamishna wa Lungalunga Josphat Biwott.
Hata hivyo serikali ya Tanzania tayari imeanza harakati za kuhakikisha kuwa raia hao wanaachiliwa huru. Naibu waziri wa uvuvi na ufugaji nchini Tanzania Abdalla Ulega ameliambia gazeti la The Citizen nchini humo kwamba juhudi zimeanza ili kuona kuwa tatizo hilo limetatuliwa.
''Tayari tumezungumza na wizara ya masuala ya kigeni na jeshi la polisi ili kuona tatizo hilo litakavyoangaziwa. Walikamatawa kulingana na sheria za Kenya'', amesema na kuongeza.
''Inapokuja katika uhalali wa vitendo vya uvuvi, kila taifa lina sheria zake ,Serikali inajua hilo'', amenukuliwa na gazeti hilo akisema
Kenya na Tanzania zimekuwa katika msururu wa mgogoro wa kibiashara ambao umekuwa ukizua uhasama katika ya mataifa hayo jirani.
Mapema mwaka huu mataifa hayo yalianza mchakato wa kuweka alama katika mipaka yake kwa kuondoa vigingi vilivyooza na kuweka vipya.
Mpaka wa Kenya na Tanzania una urefu wa kilomita 769 na hutumiwa na jamii kutoka mataifa na pande zote mbili za mpaka kufanya biashara, kilimo na ufugaji hususan miongoni mwa kabila la Wamasai.

Kulingana na Business Daily, Mbunge wa Lunga Lunga nchini Kenya Khatib Mwashetani ameomba kuwachiliwa kwa wavuvi hao akiongezea kuwa baadhi yao wanaishi nchini Kenya.
Katika siku za awali wavuvi wa Kenya wameyashutumu mataifa ya kigeni kwa kushiriki katika uvuvi haramu kwa kutumia vyombo vikubwa katika pwani ya taifa hilo.

No comments:

Post a Comment