Sunday, 10 June 2018

Polisi Moro yachunguza iwapo kulifanyika uzembe dhidi ya mahabusi aliyejifungua njianiJohn Nditi, Morogoro

POLISI mkoani Morogoro inaendelea na uchunguzi kuhusu mwanamke aliyejifungua mtoto wakati akiwa njiani kupelekwa Kituo cha Afya Mang’ula, wilaya ya Kilombero mkoani hapa.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP), Mugabo Wekwe, amesema hayo jana katika taarifa yake kwa waandishi wa habari kuhusu tukio la kujifungua mtoto njiani mwanamke Amina Mbunda (27), mkazi wa kijiji cha Kiswanywa.

Polisi inakusudia kubaini iwapo mwanamke huyu mahabusu kulikuwa na uzembe dhidi ya watendaji ama askari na ikibainika hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao.

Amesema Polisi inaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio la mwanamke huyo aliyefikishwa katika kituo cha Polisi Mang’ula kwa kosa la kukutwa na mali ya wizi kisha kujifungua akiwa njiani kuelekea katika Kituo  cha Afya Mang’ula.

Amesema , Mei 31, mwaka huu ilifunguliwa kesi ya wizi wa samani mbalimbali zenye thamani ya sh. 1,040,000 katika kituo cha Polisi Mang’ula zilizoibwa kwa vipindi tofauti katika karakana ya Joseph Mdee iliyopo maeneo ya Posta Mang’ula .

Wekwe amesema baada ya tukio hilo uchunguzi ulianza mara moja na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Ridhiwani Athuman na kukiri kuiba kisha kuwauzia watu mbalimbali akiwemo Abdallah Mohamed Mrisho (40), mkazi wa Kijiji cha Kiswanywa ,Tarafa ya Mang’ula.

Amesema ,askari walifika nyumbani kwa Mrisho kwa ajii ya upekuzi wakiwa na mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na mlalamikaji na kumkuta mke wake (ambaye ni mtuhumiwa) na kujitambulisha kisha kumweleza kuwa wanahitaji kufanya upekuzi.

Amefafanunua kuwa wakati wa upekuzi huo mlalamikaji alibaini kuwa fumbati “ base” ya mbele ya kitanda ikiwa katika kitanda kilichofungwa ni ya kwake na ilichukuliwa kama kielelezo pamoja na mwanamke huyo kwani ndiye aliyekutwa na mali hiyo ya wizi kisha kupelekwa kituo cha Polisi Mang’ula siku hiyo ya Mei 31, mwaka huu majira ya saa 12 jioni kwa hatua zaidi.

Amesema kabla ya kuondoka na mtuhumiwa huyo, Mwenyekiti wa kijiji pamoja na askari walimjulisha mume wa mama huyo kwa njia ya simu kuwa mke wake amechukuliwa baada ya kukutwa na mali ya wizi na kupelekwa kituo cha Polisi Mang’ula na dhamana iko wazi na mume wa mama huyo aliahidi kuwa atafika kituoni akitoka katika shughuli zake.

Kaimu Kamanda huyo amebainisha kuwa mume wa mama huyo hakufika kituoni hapo na hakukuwa na ndugu wala jirani aliyefika kituoni kwa ajili ya kumwona au kuomba dhamana hivyo ililazimika awekwe mahabusu kwa mujibu wa taratibu.

Amesema ilipofika saa tisa usiku mama huyo (Mtuhumiwa) alianza kulalamika kuwa anajisikia vibaya na anadhani huwenda ikawa ni uchungu ndipo askari walitafuta gari la kumpekea katika kituo cha afya na kutofanikiwa kuupata usafiri huo.

Kaimu Kamanda wa Polisi huyo amesema mmoja wa askari aliyekuwapo kituoni hapo aliamua kuchukua pikipiki yake kumbeba mama huyo pamoja na kukodi pikipiki nyingine (Bodaboda) kisha kumpakia mama mmoja aliyeishi jirani na eneo la tukio aitwaye mama Kipangula kuelekea katika kituo cha afya Mang’ula.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi huyo mara tu baada ya kutoka Kituo cha Polisi wakielekea kituo cha Afya mama huyo alilalamika kuwa anataka kujisaidia,, waliposimamisha pikipiki na mama huyo (mtuhumiwa )alishuka ndipo alipoanza kijifungua na kusaidiwa na mama Kipangula kisha kukimbizwa katika zahanati iliyokuwa jirani na eneo hilo iitwayo Lugusha na kupatiwa huduma ya kwanza.

Amesema baada ya huduma hiyo, mama huyo aliwahishwa katika Kituo cha Afya Mang’ula ambapo alipokelewa akiwa salama yenye na mtoto wake wa kike na kuendelea kupata huduma kama kinamama wengine wanaojifungua nje ya hospitali.

Katika hatua nyingine Mganga wa Kituo cha Afya Mang’ula ,Samweli Msomba akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu amesema licha ya yenye kutokuwepo siku ya tukio hilo, lakini mama huyo aliletwa katika Kituo hicho akiwa tayari amejifungua na kulazwa kwa uangalizi kwa muda wa siku tatu na baadaye aliruhusiwa kwenda nyumbani.

Amesema mtoto huyo alizaliwa akiwa na uzito wa kilo 3.5 na kwamba mama wa mtoto huyo hakuwa na tatizo baada ya kujifungua na alilazwa wodini kwa siku tatu ili kuona kama yapo madhara aliyapata wakati wa kujifungua.

No comments:

Post a Comment