Saturday, 9 June 2018

Wanawake wajasiriamali 7,000 wanufaika na mkopo wa bililioni 13/=

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu (wanne kushoto mstari wa nyuma) akiwa na viongozi wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara na wanawake wajasiriamali waliowezeshwa mikopo na asasi ya Wedac. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya asasi ya Wedac iliyotoa mkopo wa sh. bilioni 13 kwa wanawake 7,354 mjini Mbulu, Manyara.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu akimkabidhi mkopo wa sh. milioni 2.5 mjasiriamali wa mjini Mbulu, mkoani Manyara, Zahara John uliotolewa na asasi ya Wedac kulia ni mbunge wa viti maalum mkoani Manyara, Martha Umbullah.  


 Mwandishi Wetu

WANAWAKE wajasiriamali 7,354 wa wilaya za Mbulu, Monduli na Hanang’, mkoani Manyara na Arusha, wamenufaika kiuchumi kupitia mikopo ya sh. Bilioni 13.7 iliyotolewa na asasi isiyo ya kiserikali ya Wedac.

Asasi hiyo ya Wedac imewawezesha kiuchumi wanawake hao 7,354 kupitia vikundi vyao 1,471 na pia wanawake binafsi 239 wasiokuwa kwenye vikundi walijipatia mikopo ya thamani ya sh. milioni 680.3. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza mjini Mbulu, mkoani Manyara kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya asasi ya Wedac aliipongeza kwa kuwawezesha kiuchumi wanawake hao. 

Waziri Mwalimu amewataka wanawake kujishughulisha na ujasiriamali ili kujipatia kipato na wasikubali kubweteka kwa kukaa bila kazi ili kuondokana na migogoro ya kila mara na wenza wao. 

Amesema iwapo wanawake wakijishughukisha kwa kufanya ujasiriamali watapunguza migogoro majumbani mwao kwani nao watajiweza kiuchumi na kuondokana na utegemezi kwa waume zao. 

Ameipongeza asasi ya Wedac kwa kuwawezesha kiuchumi wanawake hao 7,354 kupitia vikundi vyao 1,471 kwani wanawake wakiwezeshwa jamii nzima inanufaika.

“Wedac mmefanya kazi nzuri mno kwani nimesoma taarifa yenu pia mmewapa mikopo ya mtu mmoja mmoja wanawake 239 yenye thamani ya a sh. milioni 680. 3 ambao wamejinyanyua kiuchumi,” amesema Waziri Mwalimu. 

Mshauri mkuu wa Wedac, Martha Umbullah ambaye pia ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Manyara, amesema lengo lao ni kuhakikisha wanapunguza umaskini miongoni mwa jamii. 

Umbullah amesema wamewajengea uwezo wanawake ili wajikwamue kiuchumi kwa kuwapa mikopo midogo midogo ya kuendesha biashara na kuirejesha. 

Ameongeza kuwa wanawake wamejijengea tabia ya kujiwekea akiba, yaani kabla ya kukopa anaweka akiba yake kama dhamana na anaongeza kiasi hicho kila anapokopa kwa mara nyingine. 

Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, Alexander Mnyeti ameipongeza Wedac kwa kuwawezesha kiuchumi wanawake wa eneo hilo. 

Mofuga amesema wataiunga mkono asasi hiyo kwani inashirikiana na serikali katika kuwasaidia wananchi waondokane na umaskini. 

Mjasiriamali wa Ayamohe mjini Mbulu, Mwanahamisi Salum amesema alianza kupewa mkopo wa sh. 200,000 mwaka 2015 lakini hivi sasa anachukua mkopo wa sh. milioni 2. 

Mjasiriamali Angela Stephano amesema kupitia mkopo wa sh. 500,000 aliouchukua atauendeleza mtaji wake wa biashara ya nguo na viatu uliopo mjini Mbulu.

No comments:

Post a Comment